Wednesday, November 4, 2015


WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta ametangaza kuwa atawania nafasi ya Spika ili kuliongoza Bunge la 11. Sitta aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Tisa amekuwa kada wa kwanza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kujitosa katika mchuano wa kuwania nafasi hiyo nyeti wakati huu ambao Bunge limevitaka vyama vya siasa viwe tayari kwa ajili ya kupeleka majina ya wateule wao wa nafasi hiyo mara itakapotangazwa kuwa wazi.

Msemaji wa Spika huyo mstaafu, John Dotto alisema jana Dar es Salaam kuwa Sitta amemua kuwania nafasi hiyo kutokana na uwezo na uzoefu alionao wa kuendesha Bunge. Alisema Sitta anaamini kuwa uwezo wake aliouonesha katika kuendesha Bunge la Tisa akitumia kaulimbiu yake ya ‘Spika wa Kasi na Viwango’ itamfanya aendane na kasi ya utendaji wa Rais Mteule, Dk John Magufuli.

Sitta alijizolea sifa wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, ikiwamo Bunge hilo kufanyia marekebisho ya kanuni mbalimbali zilizolifanya liwe na makali na kuibua kashfa nzito ikiwamo ya Richmond ambayo ilisababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na alilirejeshea makali Bunge.

Tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano limetangaza kuanza kwa mchakato wa kumpata Spika mpya wa Bunge, atakayerithi mikoba ya Spika Anne Makinda.
 
 Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel akizungumza na vyombo vya habari Dar es Salaam mapema wiki hii alisema kuwa mgombea wa nafasi ya Spika, anaweza kuwa Mbunge au mwanachama yeyote wa chama kwa masharti kwamba kama si Mbunge, jina lake lazima liwasilishwe kwanza Tume ya Taifa ya Uchaguzi siku tano kabla ya uchaguzi kujiridhisha kuwa mgombea huyo ana sifa za kuwa Mbunge.

Bunge hilo la Tisa lilipata ufanisi na mafanikio kadhaa kutokana na ubunifu na ujasiri wa baadhi ya wabunge wakiongozwa na utayari wa Sitta ambaye wakati akishika nafasi hiyo aliahidi kuwa ‘spika wa kasi na viwango.’

Mafanikio yaliyopatikana katika Bunge hilo ni pamoja na kutungwa kwa Kanuni mpya za Bunge za mwaka 2007, ambazo zimeelezwa kuwa zilisaidia kwa kiasi kikubwa kuliwezesha lifanye kazi kwa ufanisi kama vile kuondoa ukiritimba wa serikali kuwa ndiyo pekee inayoweza kupeleka muswada bungeni.

Kanuni hizo mpya za mwaka 2007 ambazo zilitokana na kufanyia marekebisho makubwa kanuni za Bunge za mwaka 2004, zilitoa mamlaka kwa kamati za kudumu za Bunge kuwa na uwezo wa kupeleka mswada kwa ajili ya kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwa sheria.

0 comments:

Post a Comment