Hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere akiwa na mke wake.Picha na Maktaba
Oktoba
14 ya kila mwaka Watanzania hukumbuka siku ya huzuni, ambapo
walimpoteza Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki dunia
tarehe na mwezi huo, mwaka 1999 katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas
nchini Uingereza alipokwenda kwa matibabu.
Madaktari
walieleza kuwa kifo cha baba wa taifa kilitokana na ugonjwa wa saratani
ya damu. Julius Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa Kwanza wa Tanganyika
huru na baadaye alikuwa Rais wa kwanza wa Tanganyika.
Mwalimu
alikuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania Baada ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar, ambapo alikaa madarakani akiiongoza Tanzania kwa miaka zaidi
ya 20.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII KWA KUBOFYA HAPA CHINI
Oktoba
14 ya kila mwaka imefanywa kuwa ya kitaifa ikitoa nafasi ya kumbuka,
kutafakari aliyolitendea taifa, lakini zaidi kuenzi yote mema na mazuri
kwa Tanzania aliyoipenda.
Tangu kufariki kwake mengi yamekuwa yakikumbukwa na kutajwa kama mfano na watu wa kada mbalimbali, wakiwamo viongozi.
Ni
wazi na hakuna anayeweza kupinga kuwa Mwalimu Nyerere ameacha mambo
mengi mazuri ya kujivunia na mfano wa kuigwa na jamii ya Watanzania.
Historia
hiyo ipo katika nyanja mbalimbali kama vile siasa, elimu, uchumi hata
utamaduni katika taifa la Tanzania linaloelezwa kuwa na makabila zaidi
ya 120, hivyo pia kuwa na tamaduni tofauti kati ya kabila moja na
nyingine, ingawa baadhi ya makabila hufanana mila na utamaduni wao
kwenye baadhi ya mambo.
Katika
makala haya leo, tunaangalia namna Mwalimu Julius Kambarage alivyoacha
historia ya kipekee katika kuenzi utamaduni wa kabila lake na kuheshimu
uhusiano katika familia na urafiki wake na watu wengine.
Ukweli
wa hilo unadhihirishwa na jinsi Mwalimu alivyokuwa akitoa majina kwa
watoto wake, wajukuu na jinsi alivyokuwa akiwaita kila mmoja kwa namna
yake, akizingatia uasili na heshima kati yake na watu wengine.
Ndivyo
ilivyo, Mwalimu aliwapa majina watoto wake akitaka kila mmoja awe na
jina lenye maana kama siyo kwa familia, basi kwake binafsi.
Hapa
mfano wa karibu ni namna alivyowapa majina watoto wake kwa kuwapa
majina ya pili ambayo ni ya kiasili na kwa namna tofauti, huku kila jina
likiwa na maana kwa familia na kwake.
Katika
uhai wake, Mwalimu Nyerere alibahatika kupata watoto saba ambapo mbali
na majina yaliyotokana na imani yake ya dini ya Kikristo, kila mmoja
alimpa pia jina la kiasili ya Kizanaki, kabila alilotokea, ukoo wake au
wa mkewe mama Maria Nyerere.
Akionyesha
mfano wa kuthamini uafrika na asili yake Nyerere alimwita mtoto wake wa
kwanza kwa jina la Burito au Andrew, mwingine alimwita Watiku (Anna),
Magige(Emily), Nyerere (John), Makongoro (Charles) na Madaraka ambaye ni
Godfrey.
Mmoja
wa wajukuu zake aliyempa jina la Moringe anasema kuwa anaamini kila mtu
katika familia ya mwalimu alipewa jina kwa sababu maalumu, kwani pamoja
na kuwa majina mbalimbali, bado babu yao aliwaita kwa maana ya jina la
kiasili.
Anatoa
mfano wa baba yake yeye, (Mzee Magige) ambaye alipewa jina la baba wa
Mama Maria Nyerere, hivyo Mwalimu alikuwa akimwita Magige ‘mkwe’.
“Babu
alikuwa akimwita baba yangu kwa lugha ya Kizanaki ‘Tata Kyara’
akimaanisha baba mkwe, nimemsikia akimwita hivyo siku zote na hakuwahi
kutumia jina lake la Magige au Emily.
Anasema
hata yeye alipewa jina la Moringe ambalo ni la Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Moringe Sokoine kwa sasa ni marehemu, ambaye alikuwa ni rafiki
mkubwa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
“Mimi
siku zote alikuwa akiniita ‘rafiki yangu’ kwa kuwa alinipa jina la
rafiki yake kipenzi, hakuwahi kuniita kwa jina langu la Moringe hata
siku moja,” anasema.
Anaongeza
kuwa alifanya vivyo hivyo kwa ndugu wote akiwaita kutokana na asili ya
majina yao na kwa kuwa wengi walikuwa na majina ya Kizanaki aliwaita
kutokana na uhusiano au tafsiri ya majina hayo.
Moringe
anasema kuwa Nyerere aliwalea watoto na wajukuu zake katika maisha
yaliyolenga kuwaonyesha Watanzania kuwa kila mtu ni sawa kwa kuwa pamoja
na kuwa na madaraka, hakuyatofautisha maisha yake na ya Watanzania
wengi.
“Nchi
hii matajiri ni wachache kuliko maskini, alitaka familia yake iishi
maisha ya kawaida, yanayofanana na ya Watanzania wengi ingawa alikuwa na
uwezo wa kuwafanya waishi kama wako peponi.
Hii ililenga kuonyesha kwamba alijali usawa na kutaka kila mmoja ajione muhimu katika nchi yake,” anasema Moringe.
Anabainisha
kuwa Mwalimu hakutaka Watanzania wajione wanyonge kwa tabaka na
walionacho na wasionacho na yeye alipinga hali hiyo kwa kuonyesha mfano.
“Isingekuwa
na maana kwa babu kufanya mambo ambayo kwa Watanzania ni mageni, kama
angefanya hivi pengine leo hii sisi kama familia au kama Watanzania
tusingejivunia kupata mtu kama yeye,” anasema Moringe.
Anaongeza
kuwa unapotaka kusisitiza jambo fulani lifanyike, mwenyewe unatakiwa
kuwa mstari wa mbele kuongoza mapambano na hiki ndicho alichokuwa
akifanya Baba wa Taifa.
“Kama
angejihusisha na biashara nyingine wakati akiwa kiongozi wa nchi, maana
yake angetengeneza mwanya kwa viongozi wengine kufuata nyayo zake na
hii ingeweza kutengeneza mianya ya rushwa na ukiukwaji wa maadili,”
anasema Moringe. Akizungumzia yeye kutaka kujiingiza katika siasa
anasema atafuata nyayo za babu yake ambaye kabla alitumikia taaluma yake
na baadaye ndipo akajiingiza huko.
“Ninapenda
kufuata nyayo za babu, alisoma, akawa mwalimu na baadaye ndiyo
akajiingiza katika siasa, nami nitafanya hivyo, sasa hivi ni wakati
wangu wa kuitumikia taaluma yangu mpaka pale nitakaporidhika ndipo
nitaingia kwenye siasa,” anasema Moringe.
MWANANCHI
Categories: KITAIFA
0 comments:
Post a Comment