Zaidi, kwenye mahojiano
maalumu, nyumbani kwake Tengeru, Arusha, Mtei anabashiri kuwa iwapo
kiongozi huyo angekuwa hai hadi leo, bila shaka angeachama na chama
chake alichokiasisi na kujiunga na Chadema. Endelea…
Swali: Umepata kufanya kazi na Mwalimu Julius Nyerere, hivi huyu alikuwa ni mtu wa aina gani?
Jibu:
Nilimfahamu Mwalimu mwaka 1959 mwishoni niliporudi nyumbani nikitokea
masomoni Makerere nchini Uganda. Unajua Serikali ya Kikoloni haikunipa
kazi, nikaamua kwenda Kenya kufanya kazi.
Siku moja nilikwenda kumtembelea Mwalimu nyumbani kwake nikiwa na rafiki yangu Mwanjisi, Mwanjisi ndiye aliyenipeleka.
Tulikaa tukaongea na tukafahamiana, ndipo alipotuambia kwamba ipo siku wakoloni wataondoka na sisi tutalitumikia taifa letu.
Mwalimu alikuwa ni mtu jasiri, ndiye aliyethubutu kuwaambia wakoloni waondoke, lakini hapo awali watu walikuwa wakiogopa kusema.
Yeye alisimama na kukemea ubaguzi wa aina yoyote.
Mwalimu
pia alipenda haki na usawa. Hakupenda kabisa uonevu, lakini tatizo lake
alikuwa haambiliki. Kile alichokisema alitaka hicho hicho kifuatwe,
hakupenda mtu wa kumwambia hapana.
Swali: Mwalimu Nyerere alichukia nini enzi za uhai wake?
Jibu:
Alichukia wezi wa mali ya umma na yeyote yule aliyekuwa mdokozi
alimfukuza mara moja bila kumwonea haya. Unajua, Mwalimu alipobaini
kwamba kuna mtu katika idara fulani hata wizara ni mzembe au mvivu,
alimhamishia sehemu nyingine.
Mwalimu alikuwa tayari kuhakikisha
wananchi wanamiliki rasilimali zao kama madini na wanazifaidi na siyo
kuwapa wageni. Yeye alipenda Watanzania wafaidi rasilimali zao siyo
chini ya asilimia hamsini.
Alisema wazi kabisa kwamba haya madini
yaliletwa na Mungu hayakujileta yenyewe, hivyo alipenda wazawa wazifaidi
rasilimali zao na siyo wageni.
Mimi nashangaa, baadhi ya viongozi wa
CCM wa sasa tofauti na Nyerere, hawalioni hilo. Kuna tofauti kubwa kati
yao na Mwalimu. Yeye aliwapenda watu wake lakini viongozi wa CCM
wanawachukia watu wao na kuwakumbatia wageni wanaowaita wawekezaji.
Swali: Ni tukio gani ambalo huwezi kulisahau wakati ukifanya kazi na Mwalimu Nyerere?
Jibu:
Siwezi kusahau kipindi ambacho nilijiuzulu ugavana kwani tulitofautiana
sana na Mwalimu hadi nikaamua kuuza nyumba yangu Dar es Salaam na
kuhamia Arusha, na hapa nimekuwa mkulima hadi leo.
Unajua Mwalimu
alikuwa mtu asiyependa demokrasia hata kidogo, alikuwa mtu ambaye
haambiliki, yeye alipenda kile alichokisema tu kitekelezwe.
Mwaka
1977 Mwalimu Nyerere walitofautiana na Mzee Kenyata na alifunga mpaka wa
Tanzania na Kenya, wakati huo Milton Obote (Rais wa Uganda enzi hizo)
alikuwa ameporwa madaraka na Idd Amin na ndipo Jumuiya ya Afrika
Mashariki (EAC) ikavurugika.
Mimi nikiwa ni Katibu Mkuu wa jumuiya hiyo niliamua kurudi nyumbani.
Niliporudi
nikapewa nafasi ya kuwa Waziri wa kwanza wa Fedha, wakati huo tukiwa
katika vita ya Uganda na mimi ndiye nilikuwa nikisimamia masuala ya
uchumi na fedha wakati wote wa vita. Vita ilipoisha nchi yetu iliingia
katika mtikisiko mkubwa wa kiuchumi, hatukuwa na fedha kabisa.
Ndipo
nikaamua kumshauri Mwalimu, kwamba tukope fedha katika Benki ya Dunia
ili kutatua suala hili. Baada ya kushauriana na watu wa Benki ya Dunia
nilimwambia Mwalimu pia tupunguze bajeti ya matumizi yetu, nilimshauri
vitu vingi kwa kweli.
Unajua, Mwalimu alinijibu kwamba mimi
nimeshawishiwa na watu wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), ndipo nikaamua
kujiuzulu. Huwezi kuamini na siku najizulu Mwalimu alitoa hotuba ya
kuridhia kujiuzulu kwangu na kusema kwamba ‘kamwe hawezi kuruhusu
serikali yake iongozwe kutoka Washington.’
Hakika nilishtushwa na
hotuba yake baada ya mimi kujiuzulu ukizingatia ya kwamba mimi nilikuwa
nimelitumikia taifa langu kwa uadilifu mkubwa, ndipo nikaamua kuwa
mkulima hadi leo. Niliuza nyumba yangu Dar es Salaam na kununua shamba
kubwa hapa Tengeru mkoani Arusha.
Mwalimu alipenda watu wa kumwambia
‘ndiyo mzee’ na bahati mbaya mimi sikuwa mtu wa namna hiyo. Kila
alichokisema alitaka kifuatwe na hata umma unajua kwamba mimi
nilithubutu kumwambia Mwalimu ‘hapana’.
Swali: Ni jambo gani zuri ambalo unalikumbuka kwa Mwalimu Nyerere?
Jibu:
Kwanza kabisa, yeye ndiye mwasisi wa taifa letu, alipenda sana nchi
yake na hata pia alipenda uhuru wa nchi nyingine barani Afrika. Ndiyo
maana wakati mwingine alikuwa tayari kuchelewesha uhuru wa Tanganyika
ili nchi nyingine za Afrika zipate uhuru.
Hakika, Mwalimu aliipenda
sana Afrika, alisaidia harakati za ukombozi wa nchi mbalimbali za
Afrika, alikuwa mzalendo wa kweli ambaye hakuwahi kutokea kabisa kabla
yake.
Hii nchi aliyoipigania Mwalimu ibaki moja, tusiigawe vipande
vipande. Isiwe kundi la watu fulani linapokea mapesa na wengine wanyonge
wanataabika, wanakufa na njaa. Leo tunasikia kuna vigogo wanaficha
mapesa nje ya nchi hii ni ajabu sana”.
Swali: Iwapo Mwalimu Nyerere angelikuwa hai, je, unadhani angekemea mambo gani?
Jibu: Kwanza kabla ya kukujibu, Mwalimu angekuwa hai leo nakuambia kwanza tayari angekuwa ameshajiunga Chadema.
Na tuna imani huko aliko anatupigia makofi kwa kazi nzuri tunayoifanya ya kukemea ufisadi na rushwa kama sera yake ilivyokuwa.
Unajua Mwalimu enzi za uhai wake alishawahi kutuambia mbele yangu kwamba Chadema ndicho chama mbadala wa CCM.
Ndicho chama kitakachoweza kuongoza nchi hii baada
ya CCM na leo tunaona utabiri wake. Lakini, niseme angekuwa hai
angekemea vitendo vya kukithiri kwa rushwa na ufisadi, kwani sasa
tunaona kundi la walionacho na wasionacho linavyokua hapa nchini.
Swali: Je, unadhani misingi aliyoiacha Mwalimu Nyerere inafuatwa leo hii?
Jibu: Kwanza kwa uhuru aliotupatia, hilo hakuna mtu wa kutupora. Kingine, misingi yake haifuatwi kabisa.
Mwalimu alipenda haki na usawa, maskini wapate na
matajiri wapate, lakini kwa hali ya sasa hatuna viongozi wa kukemea
rushwa wala ufisadi kwa kuwa hata wao wamechaguliwa kutokana na mkondo
wa rushwa. hiyo hiyo.
-----MWANANCHI